KARIBU KWENYE ALCOHOLICS ANONYMOUS KENYA
Uzoefu wetu katika ushirika wa A.A. umetufundisha mambo mawili muhimu: Kwanza, walevi wote, kimsingi, wanakabiliwa na matatizo yaliyo sawa – wawe ni masikini wanaopigania kupata angalau bia ndogo tu, au ni matajiri wanaoshikilia vyeo vya ukurugenzi wa mashirika makubwa. Pili, sasa tunakubali ya kwamba mpango wa uponyaji wa A.A unafanya kazi kwa karibu kila mlevi anayeazimia kwa dhati kwamba itamfaidi, bila kujali hali yake ya zamani au asilia yake au mpangilio wa unywaji aliokuwa nao.
TULICHUKUA UAMUZI
Sote tuliopo sasa katika A.A. tulilazimika kuchukua uamuzi wa mwisho kabla kujisikia tuna usalama katika mpango mpya wa maisha bila kileo. Tulilazimika kukabiliana vilivyo na ukweli juu ya hali yetu na unywaji wetu, kwa ukweli na uaminifu. Ilitulazimu kukiri kwamba hatuna nguvu dhidi ya kileo. Kwa baadhi yetu, hii ilikuwa hatua ngumu zaidi kwetu kuwahi kuchukua.
Hatukujua mambo mengi juu ya ulevi. Tulikuwa na mawazo yetu juu ya neno “Ulevi”. Tuliliambatanisha na ulevi chakari wa kupindukia. Tukifikiria kwa hakika linamaanisha udhaifu wa akili, udhaifu wa hadhi ya mtu. Baadhi yetu tulipigana vikali na hisia kwamba na sisi tu walevi. Wengine walikiri shingo upande.
Wengi wetu, hata hivyo, tulipata kupumua baada ya kufahamishwa ya kwamba ulevi ni aina ya ugonjwa. Tuliona maana ya kufanya kitu juu ya ugonjwa ambao ulitishia kutuharibu. Tuliwacha kujaribu kuwadanganya wengine – na sisi wenyewe – kwamba tungeliweza kukabiliana na kileo wakati ambapo wote ulikuwa ukielekea kwingine.
Tulihakikishiwa tangu mwanzo kwamba hakuna mtu anayeweza kutuambia kwamba sisi ni walevi. Sisi wenyewe ndio tuliopasa kukiri – sio kutoka kwa daktari, kasisi au mumeo au mkeo. Ilikuwa lazima iwe chini ya msingi wa ukweli tuliojua. Marafiki zetu huenda wakaelewa asilia ya matatizo yetu, lakini ni sisi wenyewe ambao tungeliweza kusema kwa hakika kwamba unywaji wetu umepita kiasi.
Mara nyingi tuliuliza, “Nitajuaje ikiwa mimi kweli ni mlevi?” Tuliambiwa ya kwamba hakuna masharti wala sheria za kupima ulevi. Tulijifundisha hata hivyo kwamba kulikuwepo na dalili za hapa na pale. Ikiwa tulipata kulewa wakati ambapo tulikuwa na nafasi ya kuwa watulivu, ikiwa unywaji wetu umeendelea kuwa mbaya zaidi, ikiwa hatupati tena starehe wakati tukinywa kama ilivyokuwa hapo awali – hizi, tulijifunza, zilikuwa baadhi ya dalili za ugonjwa tunaouita Ulevi. Tukichunguza upya uzoefu wetu wa unywaji na maafa yake, wengine wetu tuliweza kugundua sababu za ziada za kujua ukweli juu yetu.
Kwa kawaida kabisa, uwezekano wa maisha bila kileo ulionekana mgumu sana. Tuliogopa kwamba marafiki zetu wapya katika A.A. wangelikuwa wanyamavu au ikizidi, wawe wakakamavu kama waeneza injili. Tuligundua ya kuwa badala yake, walikuwa wanadamu kama sisi, lakini waliokuwa na uwezo maalum wa kuelewa tatizo letu – kwa kihuruma bila kuhukumiwa.
Tulianza kushangaa ni kitu gani tulichopasa kufanya ili kuwa watulivu, kwamba A.A. ingelitukarimu kiasi gani, na ni nani anayeliendesha shirika hilo, hapa kwetu na kote duniani. Mara tuligundua ya kwamba hakuna anayelazimishwa chochote katika A.A. Hakuna mtu anayelazimishwa kufuata matambiko yoyote rasmi au utaratibu wa maisha. Tuligundua pia kwamba A.A. haina ada au karo za aina yoyote; gharama za kukodisha chumba cha kukutania, viburudisho na vitabu zinafikiwa kwa changizo. Lakini hata changizo za aina hiyo sio masharti ya uwanachama.
Mara ilikuwa wazi kwetu kwamba A.A. ina usimamizi mdogo tu na haina mtu yeyote anayetoa amri. Mipango ya mikutano hufanywa na kundi la maafisa ambao kisha hujiondoa na kuitoa nafasi kwa wengine wapya. Utaratibu wa ‘Mzunguko” kama huu ni maarufu sana katika A.A.
KUKAA UTULIVU BILA KUNYWA
Vipi, basi mtu, utakuwa na utulivu bila kunywa katika ushirika kama huu usio rasmi, na ambao hauna sheria?
Jibu lake ni kwamba, mara unapoweza kukaa na utulivu bila kunywa, tunajaribu kuidumisha hali hiyo kwa kuchunguza na kufuatilia uzoefu wa ufanisi wa wale waliotutangulia katika A.A.
Uzoefu wao unatoa aina fulani ya “nyenzo” na maongozo ambayo yako huru kukubaliwa au kukataliwa, kama tupendavyo. Kwa sababu hali yetu ya utulivu bila kunywa ndio muhimu zaidi katika maisha yetu sasa, tunafikiria ni busara kufuata mitindo inayopendekezwa na wale walioonyesha kwamba mpango wa kupona ulevi wa A.A. kweli hufanya kazi.
MPANGO WA MASAA 24
Kwa mfano hatuchukui ahadi zozote, hatusemi kwamba hatuta “kabisa” kunywa tena. Badala yake hujaribu kufuata kile sisi katika A.A. tunachokiita “mpango wa masaa 24”. Tunazingatia kukaa na utulivu bila kunywa kwa muda wa sasa wa masaa 24. Tunajaribu tu kupitisha muda wa siku moja kwa wakati bila kinywaji. Tunapopatwa nah amu ya kunywa, hatushangai wala kupinga. Tunaashirisha tu hamu ya kinywaji hicho hadi kesho.
Tunajaribu kuweka fikra zetu kwa haki na kwa ukweli pale kileo kinapohusika. Tunaposhawishika kunywa – na ushawishi huo mara nyingi huondoka baada ya miezi michache ya kwanza katika A.A. – tunajiuliza ikiwa kinywaji hicho tunachofikiria kina thamani kuliko athari zote tulizopitia kutokana na ulevi wetu siku ya nyuma. Tunajikumbusha akilini mwetu kwamba tuko huru kabisa kulewa. Tukipenda kufanya hivyo, kwamba chaguo kati ya kunywa na kutokunywa ni juu yetu sisi tu. Na kwa muhimu zaidi, tunajaribu kukabiliana na ukweli kwamba, haijalishi tumekuwa na utulivu bila kunywa kwa muda gani, tunaendelea kuwa walevi – na walevi, kadiri ya tunavyojua, hawawezi tena kunywa kijamii kama kawaida.
Tunafuata kwa heshima nyingine, uzoefu wa “miamba” wa zamani wa unywaji waliofaulu. Kwa kawaida, tunafika, bila kukosa katika mikutano ya A.A. ya sehemu yetu ambayo tumejiunga nayo. Hakuna sheria yoyote inayolazimisha kuhudhuria kwetu. Wala hatulazimiki kila mara kueleza ni kwa nini tunajiepusha na kusikiliza hadithi na maoni ya watu wengine. Wengi wetu, hata hivyo, tunajisikia kwamba kuhudhuria mikutano na kukutana na wanachama wenzetu wa A.A. katika hadhara nyingine, ni muhimu kwa kudumisha hali yetu ya kutokunywa.